| Wapendwa kaka na dada zangu,
1. Siku kuu ya Umisionari Duniani tunayoadhimisha leo tarehe 22
Oktoba, inatupatia nafasi ya pekee ili kutafakari kuhusu mada: “UPENDO,
KIINI CHA UMISIONARI”
Umisionari kama usipotegemezwa na Upendo, usipotokana, yaani na
Upendo wa Ki-Mungu, unariski kujishusha na kuwa kama huduma tu ya
kijamii. Upendo ambao Mungu anatoa kwa kila mmoja unaunda roho ya
uzoefu na uenezaji wa Injili, kwa wale waipokeao wanakuwa ndio mashahidi.
Upendo wa Mungu ambao ni uhai kwa ulimwengu ni Upendo tuliopewa
katika Yesu, Neno la Wokovu, sura wazi ya huruma ya Baba wa mbinguni.
Ujumbe wa Wokovu unaweza kufupishwa kwa hiyo kwa kutumia maneno
ya Mwinjili Yohane. “Kwa hilo upendo wa Mungu umejidhihirisha.
Mungu amemtuma mwanae wa pekee duniani, ili sisi tupate uzima katika
yeye.” [1 Yh. 4:9]
Utume wa kueneza ujumbe wa Upendo huu, Yesu aliutoa kwa Mitume
baada ya ufufuko wake, na Mitume wakiwa wamebadilishwa ndani mwao
na Roho Mtakatifu katika siku ya Pentekoste, wakaanza kutoa ushuhuda
wa Bwana wao aliyekufa na kufufuka. Kutoka hapo, Kanisa linaendeleza
utume huo huo wa Kimisionari ambao unatangaza kwa waamini wote wajibu
wa daima bila kurudi nyuma.
2. Kwa hiyo kila jumuiya ya Kikristo inaalikwa kutangaza kuwa Mungu
ni Upendo. Ni katika fumbo hili muhimu la imani yetu nimependa kutafakari
katika Ensiklika “DEUS CARITAS EST” (Mungu ni upendo).
Katika upendo wake, Mungu anatoa zawadi kwa vizazi vyote katika
historia ya binadamu.
Hapo mwanzo mwanadamu alikuja kutoka mikononi mwa Muumba kama tunda
la Upendo. Dhambi ikatia kiza katika mwanadamu,ambaye ni mhuri wa
ki-Mungu.
Walipodanganywa na yule mwovu, mababu zetu Adamu na Eva, walipoteza
ule uhusiano mzuri wa kuaminika kati yao na Mungu, wakaamini kile
kishawishi cha yule mwovu aliyeamsha ndani yao ile roho ya ujuvi
(udadisi) ya kwamba Mungu yu na wivu kama binadamu hivi ana lengo
la makusudi la kuwanyima uhuru wao. Hivyo wao walichagua kufuata
uhuru wao ulio na mipaka badala ya kufuata Upendo wa bure kutoka
kwa Mungu. Hatimaye kama matokeo waliishia kupoteza furaha ya dhati
na hivyo kuonja uchungu wa mateso ya dhambi na mauti. Lakini Mungu
hakuwatupa, bali aliwaahidia wao na vizazi vyao wokovu, akaahidi
kumtuma Mwanae wa pekee, Yesu, ambaye angefunulia wazi kuhusu ukamilifu
wa nyakati, Upendo wake wa Kibaba, Upendo wenye uwezo wa kumwondoa
kila mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi na mauti.
Hivyo kwa njia ya Kristo tumepokea uzima wa milele, uzima ule ule
katika Utatu Mtakatifu. Shukrani kwa Kristo mchungaji mwema ambaye
hawaachi kondoo wapotee. Wanadamu wa nyakati zote wamepewa uwezekano
wa kumrudia Mungu Baba mwenye upendo, aliye tayari kumpokea mwana
mpotevu.
Ishara ya Upendo kama huo usio na mipaka ni Msalaba. Katika kifo
cha Msalaba cha Kristo, nimeandika katika Ensiklika.“DEUS
CARITAS EST” (Mungu ni Upendo), hapa kinafanyika kitendo cha
Mungu kujitoa mwenyewe ili kumwinua mwanadamu na kumkomboa kwa Upendo,
upendo ule wa dhati kabisa. Ni kwa njia hiyo ukweli huu unakamilika.
Na kutoka hapo ndipo inajieleza wazi upendo ni kitu gani. Kutokana
na muono huu mkristo anapata njia ya kuishi uhai wake, katika Upendo.
(Na. 12)
3. Katika vijilia ya mateso yake, Yesu aliwaachia wosia wanafuzi
wake waliokuwa katika karamu ya mwisho ili kuadhimisha Pasaka, “Amri
mpya ya mapendo MANDATUM NOVUM”. (“Amri mpya nawapeni,
Pendaneni” Yoh. 15:17).
Upendo wa kidugu ambao Yesu anawatakia “maraki” zake,
asili yake ni katika Upendo wa Kibaba wa Mungu. Kama anavyobaini
mtume Yohane: “Anayependa ametoka kwa Mungu, na anamjua Mungu”
(1Yh. 4:7). Kwa hiyo ili kupenda kama Mungu ni budi kuishi ndani
yake na katika yeye: Makazi ya kwanza ya mwnadamu ni Mungu na ni
yeye yule aishie katika yeye tu ana ule moto wa Upendo wa Mungu
wenye uwezo wa “kuutia nuru” ulimwengu. Hii ndiyo kazi
ya Kanisa katika nyakati zote. Hapa si vigumu kuelewa kuwa hamasa
mahususi ya kimisionari, kazi muhimu ya kwanza ya jumuiya ya kanisa,
ni uaminifu katika Upendo wa mungu, na hii ni kwa kila mkristo na
kwa kila jumuiya mahalia na katika kila kanisa mahalia kwa watu
wote duniani.
Ni katika kuelewa juu ya wajibu huu wa Kimisionari katika jumuiya,
ambapo jumuiya ya mitume wa Yesu inachota ule utayari wa upendo
katika kufanikisha kazi ya kuendeleza maisha ya kiutu na kiroho
katika ushuhuda, kama alivyoandika mpendwa Yohane Paulo II katika
Enjiclika “REDEMPTORIS MISSIO, “KIINI CHA SHUGHULI NZIMA
YA Kimisionari ni Upendo ambao ndio unaendeleza umisionari na ambao
ni kipimo pekee ambapo ni kwayo tu yote yapaswa kutendeka au kutotendeka,
kubadilishwa au kutobadilishwa. Ndicho kiini kinachopaswa kuongoza
kila tendo na ambacho yote yapaswa kuelekea. Iwapo yote yatafanywa
kwa kufuata dira ya Upendo au kwa kuongozwa na Pendo hakuna lisiloweza
kupendeza na yote huwa mema”. (Na. 60). Kwa hiyo kuwa mmisionari
maana yake ni kumpenda Mungu kwa dhati hadi hata kumtolea uhai.
Ni mapadre, watawa na walei wangapi hata katika nyakati zetu hizi
wametoa ushuhuda wa upendo kwa njia ya kifo kama mashahidi. Kuwa
mmisionari maana yake kunyenyekea (kujishusha) kama msamaria mwema
mbele ya shida za wengine, hasa za walio maskini na wahitaji, kwa
sababu aliye na upendo katika Kristo hatafuti faida yake mwenyewe,
bali ufalme wa Baba na kwa faida ya jirani.
Hii ndiyo siri ya mafanikio ya kazi ya utume wa kimisionari hadi
kuvuka mipaka na tamaduni ili kuwafikia mataifa na kuenea hadi miisho
ya dunia.
4. Wapendwa kaka na dada zangu, siku ya Usimionari Duniani iwe wakati
mwafaka wa kuelewa vizuri zaidi kuwa ni ushuhuda wa upendo, ambao
ni kiini cha Umisionari unaomhusu kila mmoja. Kuitangaza Injili
ieleweke kuwa si kazi ya mtu binafsi, bali ni kazi ya pamoja, ya
kila jumuiya.
Tunakuwa karibu na wale walio mstari wa mbele katika uinjilishaji
na hapa nawafikiria na kuwatambua wamisionari wa kiume na wakike,
na wengi wengineo, watoto, vijana, watu wazima ambao kwa njia ya
sala na ushirkiano wao kwa njia mbali mbali wanachangia kazi ya
kuendeleza ufalme wa Mungu duniani. Ni mategemeo yangu kwamba ushirikiano
huu ukue na utadumu daima kwa wote.
Natumia nafasi hii kupongeza kazi kubwa ya tume, ya Uinjilishaji
wa watu wote na ya mashirika ya Kipapa ya Kimisionari (PMS) ambayo
kwa juhudi kubwa yanasimamia na kuunganisha juhudi za walio mstari
wa mbele pande zote duniani katika umisonari.
Bikira Maria ambaye kwa uwepo wake pale msalabani na kwa sala zake
katika karamu ya mwisho alishiriki katika juhudi za mwanzo wa kazi
za umisionari katika kanisa, asimamie kazi zao na awasaidie waamini
katika Kristo ili wawe daima na Upendo wa kweli, ili katika ulimwengu
huu wenye kiu kabisa ya kiroho wawe chemchemi ya maji ya uzima.
Nawatakia hayo kwa moyo wangu wote, nawabariki nyote.
Kutoka Vatikano, 29 Aprili, 2006
[Sahihi],
(BENEDICTO XVI) PAPA |