| Wapendwa sana Kaka na Dada zangu!
Kazi ya Kimisionari ya Kanisa ni muhimu mwanzoni mwa Milenia ya
Tatu
1. Kazi ya Kanisa ya Umisionari Mwanzoni mwa Milenia ya tatu ni
yenye umuhimu mkubwa kama niliyokwisha kusema mara nyingi. Kama
nilivyo taja katika Ensiklika “Redemptioris Missio”
(Utume wa Mkombozi) umisionari ndio bado unaanza nasi yatupasa kujitosa
kwa moyo wote kwa ajili ya huduma yake (rej. 1). Taifa lote la Mungu
katika kila hatua ya hija yake katika historia yake linaitwa kushiriki
“kiu” ya Mkombozi (rej. Yn 19:28). Kiu hiyo ya kuokoa
roho za watu daima imekuwa ni mang’amuzi mazito ya watakatifu.
Inatosha kumfikiria, kama mfano, Mt. Teresia wa Lisieux, Msimamizi
wa Misioni na Askofu Komboni, mtume mkubwa wa Afrika ambaye hivi
karibuni nilipata furaha ya kumwinua kwa heshima ya altareni.
Changamoto za kijamii na za kidini zinazowakabili wanadamu katika
zama zetu zinawataka waamini kuchochea hamasa yao ya umisionari.
Ndiyo! Ni lazima kuzindua tena utume “kwa mataifa” kwa
ushujaa, kuanzia na utangazaji wa Kristo, Mkombozi wa kila mtu.
Kongamano la Kimataifa la Ekaristi litakaloadhimishwa Guadalajara
– Mexico mwezi ujao wa Oktoba, itakuwa fursa ya pekee kabisa
ya kukua katika utambuzi wa pamoja wa kimisionari kandokando ya
Meza ya Mwili na Damu ya Kristo.
Kanisa, linapoiizunguka altare, linatambua vizuri zaidi asili yake
na mamlaka yake ya umisionari. Kama mada ya Jumapili ya kiulimwengu
ya Misioni ya mwaka huu inavyosisitiza bayana “Ekaristi na
Misioni” haviwezi kutenganishwa. Licha ya tafakari kuhusu
kiungo kilichopo kati ya fumbo la Ekaristi na fumbo la Kanisa, mwaka
huu kutakuwa na rejea nzuri kabisa kwa Bikira Maria Mwenye heri
kwa sababu ya tukio la mwaka wa 150 wa tangu kutajwa dogma ya Bikira
Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili (1854-2004). Na tutafakari Ekaristi
kwa macho ya Maria. Tukitegemea maombezi ya Bikira Mwenye heri,
Kanisa linamtolea Kristo, mkate wa wokovu, kwa watu wote, ili waweze
kumtambua na kumpokea kama Mwokozi pekee wa mwanadamu.
Utume wa Kanisa unachota nguvu ya kiroho kwa kushiriki Mwili wake
na Damu yake
2. Nikirejea kimawazo ghorofani katika Chumba cha juu karamu ya
mwisho mwaka jana siku ya Alhamisi Kuu nilitia saini Ensiklika “Kanisa
la Kiekaristi” (Ecclesia de Eucharistia) na toka humo napenda
kuchukua sehemu kadhaa ambazo zitatusaidia, wapendwa wangu kaka
na dada, kuiishi Jumapili ya Missioni ya duniani mwaka huu kwa roho
ya Kiekaristi. “Ekaristi inaunda Kanisa na Kanisa linaitengeneza
Ekaristi” (n. 26), niliandika, nikiangalia namna gani utume
wa kimissioni wa Kanisa ni mwendelezo wa utume wa Kristo (rej. Yn
20:21) na huchota nguvu ya kiroho kutokana na ushirika wa Mwili
wake na wa Damu yake. Lengo mahususi la Ekaristi hasa ni “muungano
wa watu na Kristo na ndani yake na Baba na Roho Mtakatifu”
(Ecclesia de Eucharistia, n. 22). Tunaposhiriki Sadaka ya Ekaristi
Takatifu tunatambua kwa kina zaidi kwamba ukombozi ni kwa ajili
ya watu wote, na hivyo umuhimu wa utume wa Kanisa pamoja na programu
zake, “ambao una kiini chake katika Yesu Mwenyewe, ambaye
anatakiwa ajulikane, apendwe na kufuaswa ili ndani yake tuishi maisha
ya Utatu Mtakatifu na pamoja naye tuigeuze historia mpaka utimilifu
wake katika Yerusalemu ya mbinguni (Ecclesia de Eucharistia, n.
60).
Tukimzunguka Kristo katika Ekaristi Takatifu Kanisa linakua kama
taifa, hekalu na familia ya Mungu: Moja, Takatifu, Katoliki na la
Kitume. Papo hapo unafahamu vizuri zaidi hali yake ya Sakramenti
ya wokovu kwa ajili ya wote na ukweli unaoonekana ukiwa na muundo
kwa kihiararkia. Kwa yamkini “hakuna jumuiya ya Kikristo inayoweza
kujengwa kama haina msingi na kiini katika adhimisho la Sakramanti
Kuu ya Ekaristi” (Ecclesia de Eucharistia, n. 33; Presbyterorum
Ordinis, n. 6). Mwishoni mwa kila Misa Takatifu, padre anayeongoza
ibada anapowaaga washiriki akisema “Nendeni na amani”
wote wajisikie kuwa wanatumwa kama “wamisionari wa Ekaristi”
kupeleka katika mazingira yote zawadi kubwa waliyoipokea. Kwa yamkini,
yeyote anayekutana na Kristo katika Ekaristi Takatifu hawezi kuacha
kutangaza upendo wenye rehema wa Mkombozi kwa njia ya maisha yake.
Hitaji la mitume ambao ni “bingwa” na mashahidi katika
adhimisho la, kuabudu na kutafakari Ekaristi Takatifu
3. Ili kuishi Ekaristi Takatifu ni muhimu na pia yatupasa kutumia
muda mwingi mbele ya Sakramenti kuu kuabudu, jambo ambalo mimi mwenyewe
ninalionja kila siku ninachota humo nguvu, faraja na msaada (ref.
Ecclesia de Eucharistia, n. 25). Mtaguso wa Pili wa Vatikano unathibitisha
kwamba, Ekaristi ni “Chemchemi na kilele cha maisha yote ya
Kikristo” (Lumen Gentum, n. 11), “chemchemi na kilele
cha uinjilishaji wote” (Presbyterorum Ordinis, n. 5).
Mkate na divai, kazi ya mikono ya wanadamu, vilivyogeuzwa, kwa
nguvu ya Roho Mtakatifu, kuwa Mwili na Damu ya Kristo, vinakuwa
amana ya “mbingu mpya na dunia mpya” (Ufunuo 21:1),
inayotangazwa na Kanisa katika utume wake wa kila siku. Katika Kristo,
ambaye tunamwabudu akiwa katika fumbo la Ekaristi Takatifu, Baba
alitamka neno lake la mwisho kuhusiana na mwanadamu na historia
ya mwanadamu.
Kanisa lingewezaje kutekeleza wito wake bila kujenga uhusiano wa
kudumu na Ekaristi Takatifu, bila kujilisha na chakula hiki kinachotakatifuza,
bila kujenga utendaji wake wa kimisionari juu ya msaada huu wa lazima
kabisa. Ili kuweza kuuinjilisha ulimwengu kuna haja ya kuwepo kwa
mitume “bingwa” na mashahidi katika kuadhimisha, kuabudu
na kutafakari Ekaristi Takatifu.
Waamini hujaliwa kutambua kwamba kazi ya umisionari ni kuwa “sadaka
yenye kibali kama toleo, ikishatakaswa na Roho Mtakatifu”
4. Katika Ekaristi Takatifu tunaliweka hai fumbo la Ukombozi linalofikia
kilele katika sadaka ya Bwana, kama inavyotamkwa katika maneno ya
konsekrasio: “Mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu….
Damu yangu itakayomwagika kwa ajili yenu” (Luka 22:19-20).
Kristo alikufa kwa ajili ya wote; na kwa ajili ya wote anakuwa zawadi
ya wokovu ambao Ekaristi Takatifu inaifanya mithili ya Sakramenti
uwepo wake katika mwendo wa historia: “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka
mimi” (Luka 22:19). Amri hiyo wanakabidhiwa wahudumu walioamriwa
kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu. Watu wote wanaalikwa
kwenye karamu hii ili waweze kushiriki katika uzima ule ule wa Kristo.
“Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu,
nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi,
nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa
mimi” (Yn 6:56-57). Wakilishwa Naye waamini wanajaliwa kutambua
kwamba kazi ya umisionari ni “kuwa sadaka yenye kibali, ikishatakaswa
na Roho Mtakatifu” (Rum 15:16), ili kuwa zaidi na zaidi “moyo
mmoja na roho moja” (Mdo 4:32) na kushuhudia upendo wake hadi
mwisho wa dunia.
Kanisa, Taifa la Mungu, linaposafiri katika karne, nakurudia tena
na tena kila siku Sadaka ya Altare, linangojea ujio wa Kristo katika
utukufu. Hilo linatangazwa baada ya konsekrasiyo na Jamii inayoadhimisha,
inayoizunguka altare ikiadhimisha sadaka ya Ekaristi. Tena na tena
kwa imani iliyotiwa nguvu mpya Kanisa hurudia tamaa yake ya kukutana
hatimaye na Yule anayekuja kuleta utimilifu wa mpango wake wa kuwaokoa
watu wote.
Roho Mtakatifu akitenda kazi bila kuonekana, lakini kwa nguvu,
anaongoza taifa la Kikristo katika hija hii ya kiroho ambamo kwa
hakika wanapambana na magumu na wanaonja fumbo la Msalaba. Ekaristi
Takatifu ni kitulizo na amana ya ushindi wa mwisho kwa wale wanaopambana
na uovu na dhambi. Ni “mkate wa uzima” unaowashikilia
wale ambao Nao, kwa zamu yao, wanakuwa “mkate uliomegwa”
kwa ajili ya wengine wakilipia maisha yao hata kwa kifodini uaminifu
wao kwa Injili.
Fursa ya kuimarisha juhudi yao ya kimisionari
5. Mwaka huu, kama nilivyokwishadokeza, itakuwa ni kumbukumbu ya
mwaka wa 150 tangu dogma ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili
ilipotangazwa. Maria “alikombolewa kwa namna ya pekee na ya
hali ya juu kwa sababu ya mastahili ya Mwana wake” (Lumen
Gentium, n. 53). Nilisema katika Ensiklika “Ecclesia de Eucharistia”:
Tunapomtazama Maria, tutajaliwa kujua nguvu ile inayogeuza iliyomo
katika Ekaristi Takatifu. Ndani ya Maria tunauona ulimwengu ukifanywa
upya katika pendo” (n. 62).
Maria, “tabernakulo” ya kwanza katika historia”
(n. 55) anatuonyesha na anatupatia Kristo aliye Njia, Ukweli na
Uzima (rej. Yn 14:6). Kama Kanisa na Ekaristi Takatifu vinavyounganika
hivi bila kutengana, hayo hayo lazima yasemwe juu ya Maria na Ekaristi
Takatifu” (Ecclesia de Eucharistia, n. 57).
Natumaini kule kuingiliana kwa furaha kwa Kongamano la Kimataifa
la Ekaristi na kumbukumbu ya miaka 150 ya tangazo la dogma ya Bikira
Maria Kukingiwa Dhambi ya Asili, kutoe kwa waamini, parokia, na
asasi za kimisionari fursa ya kuimarisha juhudi zao za kimissionari
ili katika kila jumuiya iwepo daima “njaa ya kweli kwa ajili
ya Ekaristi Takatifu (Ecclesia de Eucharistia, n. 33).
Hii pia ni fursa nzuri kutaja mchango unaotolewa kwa ajili ya utume
wa Kanisa. Ninaviweka vyama hivyo kwa upendo moyoni mwangu na ninavishukuru,
kwa niaba ya wote, kwa ajili ya huduma zao nzuri zinazotolewa kwa
ajili ya uinjilishaji na utume “kwa mataifa”. Ninawaomba
nanyi kuvisaidia vyama hivyo kiroho na kwa hali a mali ili kwa njia
ya mchango wao utangazaji wa Injili uweze kuwafikia watu wote wa
hapa duniani.
Kwa hisia hizo, kwa maombezi ya Kimama ya Maria, “Mwanamke
wa Ekaristi”, kwa furaha ninawapa Baraka yangu ya Kitume.
Kutoka Vatikano, 19 Aprili 2004
Yohane Paulo II |